SIMULIZI: BUASHARA YA KIFO SEHEMU YA TATU



Peter alitoa simu yake mkononi na kumpigia Malkia. Alipewa maagizo ya kuikagua nyumba ya Richard kuona kama kuna lolote watakalolipata.
Kwa mwendo wa tahadhari, bastola ikiwa kaitanguliza mbele aliingia katika nyumba ya Richard.

*****

Huko hospitali hali ya Martin Hisia bado ilikuwa si nzuri. Ingawa sasa alikuwa anapumua bila mashine lakini bado fahamu zake zilikuwa hazijarejea.
Martin Hisia alikuwa hana fahamu wakati rafiki yake kipenzi akiuwawa nyumbani kwake. Mzimu mbaya waliofurahi kuushinda katika operesheni ngumu kabisa ya Mkanda wa Siri sasa ulikuwa umerejea. Tena umerejea kwa nguvu zote na ukiwa na hamu ya kulipa kisasi.

Chanzo Cha Haya Yote.

Martin Hisia, Brown, Binunu na Richard waliingia katika vita ya akili kupambana na wakina Malolo, Malkia na Peter ili kuupata Mkanda wa siri miaka mitatu iliyopita. Ni Mkanda uliokuwa na siri za mahali ambapo kulikuwa na madini pamoja na kiwanda cha madawa ya kulevya cha Chifu. Mwishowe kwa kushirikiana na wanajeshi wakina Martin walifanikiwa kuirudisha mali ya Serikali mikononi mwa Serikali. Na kusababisha wakina Malkia kufungwa kifungo cha maisha jela….

Maisha ya gerezani hayakuwa magumu sana kwa kina Malkia. Wote walikuwa ni watu waliozoea shurba na mateso. Maisha ya jela kwao yalikuwa laini sana zaidi ya maisha magumu waliyopitia. Wakina Malolo walikuwa watemi siku ya kwanza tu kuingia gerezani kwa upande wa wanaume. Malkia alikuwa moto siku ya kwanza tu kuingia katika gereza upande wa wanawake.
Hakuna aliyewatisha. Walikuwa wanatumikia kifungo cha maisha lakini wote waliamini ipo siku isiyo na jina watatoka kwa njia yoyote ile. Waliamua kutulia gerezani ili kuweka mipango yao sawa…

Mbozi, jijini Mbeya.

Mbozi ni miongoni mwa mji maarufu katika mkoa wa Mbeya. Pamoja na mambo mengi mazuri, lakini Mbozi ilikuwa inavuma sana kwa tabia ya uchunaji ngozi za binadamu.

Ngozi za binadamu zilikuwa dili bila ya kujulikana ngozi hizo zinatumika kwa kazi gani. Amani ilitoweka Mbozi kutokana na biashara hiyo haramu, biashara ambayo kwa kiasi kikubwa ilihusishwa na imani za kishirikina.

Ni mwaka sasa tangu mtu aitwaye Don Genge awasili katika mji wa Mbozi.
Don Genge alikuwa ni jambazi sugu aliyevuma sana miaka mitatu iliyopita. Don Genge alipeleka kizazaa kikubwa sana Kilwa miaka hiyo na kutokomea kusikojulika.

Don Genge kwa kushirikiana na mtandao wa wahalifu wa kimataifa walikuwa na mkataba wa kupeleka mioyo ya binadamu. Mioyo ambayo ilikuwa inatumika kutengenezea sumu ghali na hatari zaidi duniani. Sumu ya proxine. Biashara hiyo haramu ya mioyo ilimfanya Don awe wakala wa kupeleka mioyo. Huku mkurugenzi wa biashara hiyo nchini akiwa ni mtu aliyejulikana kwa jina la Kifo.

Siku Ile Ilikuwa Hivi.

Baada ya kambi ya kundi hatari la Six killers kuvamiwa na askari, wakiongozwa na mpelelezi mahiri nchini Tanzania, Daniel Mwaseba. Don Genge aliruka soti kinyumenyume na kuingia ndani ya nyumba yao. Alipofika ndani alisimama wima na kugeuka kwa haraka. Akili yake ilifanya kazi harakaharaka. Akili ilimwambia aende chumba cha tatu upande wa kushoto. Alikimbia mbio na kuingia chumbani. Huko ndani alikuwa anatazamana na kitanda kidogo na kabati la chuma lililowekwa ukutani. Kwa haraka alilifungua kabati na kujitosa ndani yake.

Lile kabati la chuma kwa nje lilionekana ni kabati la kawaida. Lakini ukweli lile halikuwa kabati. Lilikuwa ni zaidi ya kabati. Kabati la kazi.

Don alivyoingia mle ndani alivuta kamba ndogo ya bluu iliyekuwepo juu ya kabati lile. Kwa ndani kabati lilifunguka tena. Alijitosa ndani mzimamzima.

Lile kabati lilikuwa njia. Njia ya siri kuweza kumtoa nje ya nyumba ile iwapo mambo yatakuwa magumu. Kama hali ilivyo sasa. Ulikuwa ni mlango ambao Don Genge pekee ndio alikuwa anaufaham. Alipofika kwa ndani alivuta kikamba kingine cha rangi nyeusi kwa juu, ambacho kiliruhusu kabati kujifunga.
Kule kwa ndani alikutana na njia ndefu iliyokuwa inamtoa katika nyumba ile ambayo ilikuwa imevamiwa na mpelelezi mahiri Daniel Mwaseba na wenzake.

Wakati wakina Daniel Mwaseba wakiingia ndani ya nyumba ile kupekua, Don Genge alikuwa anafungua mfuniko wa chuma ili kuweza kutoka shimoni. Hiyo ilikuwa karibu na pwani ya Jimbiza.

Alivyotoka shimoni. Alichukua simu yake na kumpigia Kifo. Alimueleza kila kitu jinsi mambo yalivyoharibika. Saa moja baadae alikuwa juu ya ndege binafsi akielekea jijini Dar es salaam. Huku akiwaacha washirika wake toka kundi la Six killers wakiwa chini ya mikono ya dola.

Don alijichimbia miezi tisa mifichoni ili mambo aliyoyasababisha yapoe. Alikuwa anapata kila kitu katika moja la jumba la kifahari lililokuwa linamilikiwa na Kifo. Na katika kipindi hiko chote ambacho Don alikuwa mafichoni, Tanzania ilikuwa salama.
Mpaka hivi juzi tu ndipo lilipotokea tukio la hatari baada ya mtu mmoja kuchunwa ngozi huko Mbozi.

Ilikuwa ni muendelezo wa mipango haramu ya Don Genge kwa kushirikiana na Kifo kupata pesa. Walikuwa tayari kufanya lolote lile ili kuweza kupata pesa. Kuua kwao lilikuwa jambo dogo sana. Kuua kikatili ilikuwa ni burudani nzuri sana kwao.

Katika kufanya hayo, Don Genge alihitaji washirika. Sasa hakuhitaji huduma ya Six killers ambao walionesha udhaifu mkubwa sana katika misheni ya awali. Katika utafiti wake ndipo alisikia habari kuhusu Malkia na genge lake na vurugu lao katika Mkanda wa siri. Aliridhika na uwezo wao wa nguvu na akili. Don Genge alitafuta namna ya kuwatoa wakina Malkia gerezani ili aje kushirikiana nao katika biashara ya kifo..

Haikuwa kazi rahisi hata kidogo. Maana kabla ya kuwatoa wakina Malkia ilimpasa kumtafuta mtu wa kuweza kuongea nao ili kuona kama wako tayari kushirikiana na Don Genge uraiani.

Huyo mtu ilimpasa kwenda gerezani ili kuweza kuongea nao wakina Malkia.
Waelewane, kisha wawatoe.

Baada ya kuwaza na kuwazua, kichwani kwa Don Genge lilikuja jina moja tu, Devil.
Devil alikuwa kijana hatari sana katika misheni za kijasusi.

Baada ya kuongea na Devil, wiki tatu baadae wakina Malkia walikuwa nje ya gereza. Devil alitumia pesa, akili na bastola ili kufanikisha wakina Malkia wawe nje ya gereza.

Devil alitumia pesa zaidi ya milioni ishirini. Alitumia akili kuwashawishi wakina Malkia wakubaliane nao na mpango wao haramu.

Devil Ilimpasa kufanya kosa ili afungwe kuwa karibu na wakina Malkia. Aliwaambia wakamuelewa.
Risasi toka bastola ya Devil ziliua askari wapatao kumi na sita, na kuacha taharuki kubwa sana gerezani. Wakina Malkia na Devil walitoka nje ya gereza usiku wa manane, huku Devil akiwa ameahidiwa milioni hamsini.
Lakini hakuzipata!

Don Genge hakuona sababu ya kutoa hela zake bure ilhali watu akiowahitaji walikuwa mbele yake. Pia alijua kumpa hela Devil na kumuacha hai ni kufanya siri zao kuwa sio siri tena. Alimuua Devil kwa siri na kumfukia nyuma ya nyumba yake. Hakuuona umuhimu tena wa kuwa na Devil. Na safari hii alikuwa makini kuliko wakati wowote ule. Hakutaka kuruhusu kufanya kosa lolote, ndio maana aliamua kuwachukua watu makini.

Kazi ya kwanza ya kuchuna ngozi ya mtu Don Genge alifanya kwa mkono wake. Hiyo ili kuondoa dhana kwa wakina Malkia labda yeye haiwezi kazi. Na leo hii Don Genge alikuwa mbele ya wakina Malkia akiwapa kazi ya kufanya.

Don Genge alikuwa mbele ya meza. Alikuwa anatazamana na watu watatu. Malkia akiwa katikati, upande wa kushoto wa Malkia alikuwa amekaa Malolo, na upande wa kulia kwake kulikuwa na Peter Mwendawazimu. Wote macho yao yalikuwa kwa Don Genge. Walikuwa kimya wakimsikiliza bosi wao mpya.

“Naitwa Don, Don Genge. Nitakuwa mkuu wenu katika misheni hii. Najua kijana Devil ameshawaambia nini tunakusudia kufanya toka mpo gerezani.
Lakini kwa kifupi, tunahitajika kuwa makini sana katika misheni hii, kutokuwa makini ni kuikaribisha hatari”. Don Genge alinyamaza, aliwaangalia wale washirika wote, wote walionesha umakini mkubwa kumsikiliza.

ITAENDELEA…

Kama una maoni tuandikie maoni yako kwenye sehemu ya comment au wasiliana na sisi

0746587701

Tangaza nasi kwa kudhamini ukurasa huu wa simulizi piga simu namba 0746587701

Post a Comment

0 Comments