“Nawasikiliza” Don Genge aliwastua.
“Sisi tumetoka nyuma ya nondo juzi tu. Bado hatujajua kama watu tuliowaacha uraiani wana ubora uleule. Ngoja tufanye uchunguzi tutakupa jibu mkuu” Peter aliwajibia wenzake.
Don Genge alikubali kwa kuitikia kwa kichwa.
“Mkuu mimi nina swali” Peter alisema.
Don Genge alimruhusu kwa kumuoneshea mkono.
“Sisi mkuu wetu wewe, wewe mkuu wako ni nani? Yaani nani ndiye country director wa this mission?” Peter aliuliza huku akimwangalia Don usoni moja kwa moja.
“Kifo!” Don Genge alijibu kwa kifupi.
“Kifo?” Wote watatu waliuliza kwa pamoja kwa sauti ya juu.
Don Genge alikaa vizuri kitini. Aliongea huku akimwangalia Peter “Ndio anaitwa Kifo, yeye haoni shida kumuua yeyote anayeenda kinyume na mipango yake. Ameua watu wengi sana. Na hiyo ndiyo sababu ya kupewa jina hilo. Hivi juzi tu alikuwa gerezani, kwenda kuwaua Six killers baada ya kukwamisha mipango yake. Jamaa anaitwa Kifo, na anaua kweli!” Don Genge alisema kwa hisia.
“Kifo? Jina lake halisi ni nani?” Peter aliuliza tena bila ya kubabaika. Kama Don Genge alisema vile kwa lengo la kuwatisha, basi alifeli.
“Peter Genious, utafanya nini baada ya kulijua jina lake halisi?” Don Genge aliuliza.
“Sina kawaida ya kufanya kazi na mtu nisiyemfahamu. Lazima nimjue bosi wako. Kwa maana ya bosi wetu na sisi pia. Ni katika principle zangu tu nilizojiwekea tangu na tangu” Peter alisema kwa kujiamini.
“Ni siri Peter. Kila kitu hakiwezi kuwa wazi kama unavyofikiria. Hizi ni misheni za siri, acha mambo mengine yabaki kuwa siri” Don Genge alisema.
“Mbona mimi wewe unanijua, mbona wewe mimi nakujua. Nakujua kwa sura, nakujua kwa jina. Kwanini bosi wako awe siri? Yeye ana upekee gani? Nitajie jina lake ili tufanye kazi. I repeat its my principle !” Peter alisema kwa sauti kubwa.
Don Genge alikaa kimya. Alitafakari. Aliona utofauti mkubwa sana kati ya vijana wake wa zamani wa Six killers na hawa waliokuwa mbele yake. Six killers walikuwa sio watu wa kuhoji sana. Walikuwa ni watu wa ndio tu. Hawa walikuwa watu wa kujadili, watu wa kudadisi, watu wa kuuliza, kutoa maoni. Na huyu Peter alikuwa anauliza vitu vya ndani kabisa.
Pamoja na yote hayo bado Don Genge hakutaka kumtaja Kifo ni nani?
“Daaah niseme ukweli tu kwa sasa siwezi kukutajia jina lake halisi. Labda nikamuulize mwenyewe kwanza nione kama ataridhia” Don Genge alisema akiwa amenywea.
“Ukamuulize mwenyewe? Ukamuulize wapi? Wakati kikao hiki anasikiliza kila kitu. Na anatuona. Najua hivi sasa anasikia nahitaji nini, naomba akupigie simu tu na kujibu nilicho…” Peter hakumalizia kusema.
Simu ya Don Genge iliita.
Katika kioo cha simu yake lilitokea jina moja tu, Kifo. Don Genge alitetemeka kidogo. Aliipokea simu.
“Nambie mkuu” Don Genge alisema katika hali ya uwoga.
“Naona mnasumbuana na Peter. Huyo jamaa inaonesha ni mtata sana”. Kifo alisema simuni.
” Tena zaidi ya sana” Don Genge alijibu.
“Hebu mpe simu niongee nae” Kifo alisema.
Don Genge alinyoosha mkono na kumkabidhi simu Peter.
Bila ajizi Peter aliipokea.
“Mkuu” Peter alisema pindi tu alipoipokea simu.
“Naitwa Kifo!” Sauti simuni ilisema.
Peter alibabaika kidogo. Aliitambua sauti aliyoongea nayo. Aliisikia sana katika masikio yake. Tena mwisho jana tu aliisikia wakati akiangalia taarifa ya habari. Na alimuona pia.
“Nishakutambua” Peter alisema kwa kujiamini.
“Your a Genious Peter!” Kifo alisema kwa hamasa.
Simu ikakatwa.
Macho sita pale mezani yalikuwa yanamuangalia Peter. Macho yakiwa katika mshangao na udadisi.
Baada ya sekunde kadhaa, macho ya Malkia yalisafiri hadi kwa Don Genge.
Kwa mara ya kwanza alimuona Don Genge akitabasamu tangu amfahamu.
Malkia nae alitabasamu. Alijiona ni mwenye bahati sana kujuana na Peter, mwenye bahati kubwa kujuana na Malolo. Wote walikuwa na vipaji vya pekee katika nyanja zao. Hawakuwahi kumuangusha hata sekunde moja.
“Wewe jamaa wewe, kiboko aisee” Don Genge alisema huku akimpa mkono Peter.
Baadae, Don Genge alifunga kikao kwa ajili ya utekelezaji wa biashara yao ya kifo…
Nusu saa baadae Peter, Malolo na Malkia walikuwa chumbani kwa Peter.
Walikuwa wanaweka mipango yao sawa kabla ya kuingia kazini. Peter alikuwa ameshawaambia wenzake juu ya mtu mwenye sauti aliyoisikia.
Waliijadili na kuijadili.
“Hivi mnaonaje tukiwakomesha wale jamaa kabla hatujajikita kwenye hii kazi?” Malolo alichokoza mada nyingine.
“Jamaa gani tena hao Malolo?” Peter aliuliza.
“Wale jamaa wa Mkanda wa siri” Malolo alisema.
“Umesema kitu muhimu sana. Wale jamaa walijifanya wajanja sana. Lazima tuwatafute. Lazima tuwaoneshe, lazima tuwaue”. Malkia alisema kwa hasira.
“Unajua wale majamaa wana akili sana, lazima nasi tutumie akili kama tuna nia kweli ya kuwaua. Maana kupambana na Martin Hisia yahitaji uwe na zaidi ya akili” Malolo alisema.
“Tufanye hivi, tumwambie Don kwamba kuna zana zetu za kazi inabidi tuzifuate Dar. Atupe private jet moja na sumu kidogo , tukawaoneshe!” Malolo alitoa maoni yake.
“Mmmh anaweza kutupa kweli proxine kwa ajili ya kwenda nazo Dar?” Malolo aliuliza.
“Tumwambie ni kwa ajili ya kujilinda” Malkia alisema.
Saa tatu baadae Malkia, Peter na Malolo walikuwa katika jiji la Dar es salaam. Walipofika Dar walijigawa ili waifanye kazi yao kwa ufanisi.
Usiku ulimkuta Peter Magomeni. Usiku huohuo ulimkuta Malolo Tandika na Malkia Tegeta. Kila mmoja akiwa na sura ya bandia, sauti ya bandia, mwendo wa bandia na jina la bandia.
Malkia alikuwa na sura ya bandia ya msichana mrembo sana. Sauti ya bandia huku akijitambulisha kwa jina la bandia, Sophia.
Na kwa bahati mbaya kabisa Malkia ndiye aliyekutana na Martin Hisia katika baa moja huko Tegeta. Na kwa bahati mbaya tena Sophia hakuwa na sumu. Sumu walikuwa nazo wakina Malolo. Ndipo alipomlaghai Martin ili wakutane Posta. Kilichotokea huko Posta kimemfanya Martin alazwe hospitalini hadi leo. Huku Malolo akikutana na Richard mchana. Kumpasua vibaya kwa kutumia bastola yake
Jioni ya siku ya pili wakina Malkia walirejea Mbozi, Mbeya na ndege yao ya binafsi. Waliridhika kwa kazi waliyoifanya. Waliamini wamemuua Martin. Waliamini wamemuua Richard na walipata taarifa kwamba mzungu Brown alikuwa amerejea kwao Uholanzi. Sasa walikuwa tayari kurudi Mbozi na kwenda kuifanya kazi, kazi ambayo ni biashara, biashara ya kifo.
*****
Wiki moja baadae Mbozi ilikuwa katika kurasa za mbele katika magazeti yote nchini Tanzania. Mbozi ilikuwa katika habari ya kwanza katika kila stesheni ya runinga. TBC iliizungumzia Mbozi, Channel Ten waliijadili Mbozi, Star Tv waliistikia Mbozi. Mbozi iligeuka na kuwa gumzo katika redio zote Tanzania. Si radio one, clouds FM wala Times FM, zote ziliizungumzia Mbozi. Mbozi ilizungumzwa zaidi mitandaoni. Facebook, WhatsApp na Instagram iliizungumzia Mbozi.
Watu ishirini na saba walikutwa wamekufa, wengine walikutwa wamekufa majumbani kwao, wengine walikutwa wamekufa mitaani, wengine walifikwa na umauti katika nyumba za starehe. Kufa watu ishirini na saba haikuwa sababu ya habari hiyo kupewa kipaumbele katika vyombo mbalimbali vya habari, wala katika mitandao ya kijamii. Sababu ya vifo hivyo ndivyo vilivoipa uzito habari hiyo. Maiti zote zilikutwa hazina ngozi! Ilikutwa miili ikiwa nyama tupu, bila ngozi hata chembe!
Hali hiyo ilizua hofu kubwa sana huko Mbozi, pamoja na jiji la zima la Mbeya kwa ujumla.
Vifo vya watu waliochunwa vilileta taharuki kubwa sana. Watu waliogopa pasi na kawaida.
Watu walibadilisha ratiba zao za matembezi. Saa kumi na mbili jioni ikawa ni nadra kumuona akirandaranda hovyo. Walioendelea kuzurura ni kwa wale waliokuwa hawazipendi ngozi zao. Hawaupendi uhai wao. Wamechoka kuishi. Wanapenda kuzikwa wakiwa hawana ngozi.
Kati ya hao wengi wao walikuwa walevi wasioweza kuishi bila kunywa pombe. Wasioweza kulala bila kutia hata tone la pombe. Yaani ni lazima wao waende kilabuni kunywa pombe katika hali yoyote ile.
Jeshi la Polisi nalo liliingia kazini. Polisi walikuwa wanapeleleza nini chanzo cha vifo vya watu ishirini na saba waliochunwa ngozi.
Pamoja na kufanya kazi mchana, pamoja na kufanya kazi usiku, lakini Jeshi la Polisi hawakupiga hatua yoyote ile. Watu waliokuwa wanafanya mauaji hayo ya kikatili walikuwa wanatumia zaidi ya akili. Akili ambazo askari Polisi zilikuwa ni juu ya uwezo wao.
Alikuwa ni kijana mrefu, rangi ya ngozi yake ni maji ya kunde. Siku zote kichwani alikuwa anajua mtindo wa panki uliokuwa unampendeza sana. Alikuwa na kifua cha mazoezi. Mikono ya kupigana. Kichwa cha kufikiria na kuchambua mambo mbalimbali yanayohusu uhalifu. Alikuwa ana mke mmoja, mwanamke wa kinyiramba toka Singida. Wakati yeye alikuwa Mhaya toka mkoani Kagera. Alijaliwa kupata watoto wawili mapacha, wote wa kike. Alimpenda mkewe, aliwapenda watoto wake. Alikuwa anaitwa John Kashangaki, kabla ya kupanda vyeo mbalimbali katika jeshi la Polisi na kuuvaa uinspekta.
Kwa sasa jina la John Kashangaki lilifutika kabisa katika midomo ya watu na kuzaliwa jina jipya, Inspekta John.
Na huyo…..Inspekta John Kashangaki wa kituo cha Polisi Mbozi ndiye alikuwa na jukumu gumu la kupeleleza juu ya mauaji ya kikatili ya watu waliochunwa ngozi.
Ni zaidi ya siku sita sasa tangu apewe kazi hiyo, lakini hakupiga hatua yoyote ile kujua chanzo cha vifo hivyo. Alipita katika familia zote za wafiwa, lakini hakuna lolote la maana alilolipata ili kumsaidia katika upelelezi wake.
Kitu ambacho alikuwa hakijui Inspekta John kila alikokuwa anapita nyuma yake kulikuwa na mtu. Mtu ambaye walipita wote katika nyumba zote ishirini na saba. Kama Inspekta John alikuwa anapeleleza, basi na yeye alikuwa anapelelezwa, tena anapelelezwa kwa siri kubwa sana.
ITAENDELEA.

0 Comments